Updated Saturday, March 18, 2017

Museveni aagiza kuwekwa CCTV Uganda baada ya kuuawa Msemaji wa Polisi


Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameagiza kamera za CCTV zitundikwe katika miji mikubwa na barabara zote kuu za nchi hiyo, kufuatia mauaji ya Msemaji wa Jeshi la Polisi wa nchi hiyo jana Ijumaa.

Sambamba na kulaani mauaji hayo, Rais Museveni ametoa agizo hilo la kufungwa CCTV katika maeneo muhimu ya nchi, hatua inayotazamiwa kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama nchini humo.

Naibu Inspekta Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda Felix Kaweesi alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana Ijumaa ya jana. Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, Kaweesi ambaye pia ni Msemaji wa Polisi aliuawa baada ya gari lake kumiminiwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa anaondoka kwake nyumbani Kulambiro, Kisaasi kaskazini, mashariki mwa mji mkuu Kampala,
ambapo aliuawa pamoja na walinzi wake wawili walioandamana naye.

Habari zaidi zinasema kuwa, Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi wa Uganda alikuwa njiani kwenda kuwahutubia wanafunzi katika chuo kikuu cha Uganda Christian University alipokumbana na mauti yake.

Vyombo vya usalama katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki vimeanzisha uchunguzi kubaini kiini na wahusika wa mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Luteni Jenerali Henry Tumukunde, afisa mwandamizi wa jeshi la polisi la Uganda, visa vya wahalifu kufanya mauaji na jinai nyingine wakiwa juu ya pikipiki na kisha kutoroka eneo la tukio vimekithiri mno nchini humo. 
Museveni aagiza kuwekwa CCTV Uganda baada ya kuuawa Msemaji wa Polisi Museveni aagiza kuwekwa CCTV Uganda baada ya kuuawa Msemaji wa Polisi Reviewed by Bill Bright Williams on 8:50:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.