Updated Sunday, February 26, 2017

Malaysia: Kiasi kikubwa cha kemikali ya neva VX kilitumika kumuua Kim Jong Nam


Waziri wa Afya wa Malaysia, Subramaniam Sathasivam, amesema kiwango cha kemikali hatari aina ya VX inayoathiri mfumo wa neva kilichotumika kumuua Kim Jong Nam kilikuwa kikubwa sana kiasi cha kumuathiri mwili mzima.

Kim Jong Nam, ambaye ni kaka wa kambo wa Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alishambuliwa Februari 13 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur nchini Malaysia.

Waziri Sathasivam jana Jumapili aliwaambia waandishi wa habari kuwa vipimo vya baada ya kifo vimebaini kuwa moyo, mapafu pamoja na viungo vingine vya ndani ya mwili wa marehemu vilikuwa vimeathiriwa na kemikali hiyo hatari.

Alisema miligramu 10 za kemikali hatari ya VX zingeweza kusababisha kifo na kuwa anadhani kiwango halisi kilichotumika kumshambulia Kim Jong Nam kilikuwa kikubwa zaidi ya hicho. Aliongeza kusema kuwa anafikiri Kim Jong Nam alifariki katika kipindi cha dakika 15 hadi 20 baada ya kushambuliwa.

Polisi nchini Malaysia wamesema washukiwa wote wawili wa shambulizi hilo ambao ni wanawake, mmoja raia wa Indonesia na mwingine raia wa Vietnam, wameonyesha dalili za kuathiriwa na kemikali hiyo, ikiwa ni pamoja na kutapika na kuumwa kichwa.

Polisi watapokea majibu ya vipimo vya baada ya kifo juma hili na watapeleleza zaidi jinsi Kim Jong Nam alivyoshambuliwa kwa kemikali hiyo hatari.
Malaysia: Kiasi kikubwa cha kemikali ya neva VX kilitumika kumuua Kim Jong Nam Malaysia: Kiasi kikubwa cha kemikali ya neva VX kilitumika kumuua Kim Jong Nam Reviewed by Bill Bright Williams on 10:52:00 PM Rating: 5
Powered by Blogger.