Updated Wednesday, August 10, 2016

Zambia kupiga kura ya kumchagua Rais Alhamis hii


Nchi ya Zambia, Alhamisi ya wiki hii itapiga kura huku ikikabiliwa na hali mbaya kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa kampeni, ambapo Rais Edgar Lungu anapambana kusalia madarakani baada ya kupata ushindi finyu kwenye uchaguzi wa mwaka jana.

Lungu, ambaye alipata ushindi kwenye kiti cha urais kwa kupata chini ya kura elfu 28 baada ya mtangulizi wake Michael Satta kufariki, alichukua ofisi huku uchumi wa taifa hilo ukiwa matatani.

Mpinzani wake mkubwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu, Hakainde Hichilema, mfanyabiashara mwenye utajiri anayedai kuwa wizi na udanganyifu kwenye uchaguzi uliopita vilimnyima ushindi mwaka 2015, amefanya kampeni za kufa na kupona kutaka nafasi ya Urais akijaribu kwa mara ya 5.

Wafuasi wa chama cha Rais Lungu cha Patriotic Front (PF) na wale wa Hichilema wa chama cha United Party for National Development (UPND), mara kadhaa wameripotiwa kukabiliana na hali iliyosababisha kusimamishwa kwa kampeni kwa muda wa siku 10 kwenye jiji la Lusaka, mwezi uliopita.

Rais Lungu alitoa msimamo mkali wakati wa kampeni zake, huku akitoa vitisho dhidi ya mwanaharakati yeyote atakayejihusisha na kuchochea vurugu katika nchi ambayo ina amani na siasa tulivu kwa miongo kadhaa.

"Kama watanisukuma, nitahatarisha demokrasia kwa amani," Rais Lungu aliyasema haya kwenye mkutano wake wa hivi karibuni kwenye mji wa Copperbelt, mji muhimu kwa pande zote mbili kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Wakati huu matokeo ya kura ya uchaguzi yakiwa hayaeleweki, Rais Lungu amekuwa akituhumiwa kwa kujaribu kuminya upinzani kwa kuwazuia kufanya kampeni zao kwa uhuru.

-'Hofu ya kutokea vurugu' -

Mgombea mwenza wa upinzani kwenye nafasi ya urais, Godffrey Mwamba, alikamatwa na baadae kuachiwa zaidi ya mara mbili mapema mwaka huu, huku nyumba yake ikivamiwa na Polisi kwa tuhuma kuwa wafuasi wa UPND waliharibu picha za mgombea wa chama tawala.

Polisi walimuua mwanaharakati mmoja mwezi uliopita baada ya chama kikuu cha upinzani kukataa kuahirisha mkutano wake jijini Lusaka.

Gazeti maarufu nchini humo la The Post, nalo lililazimishwa kufungwa mwezi June kutokana na madeni ya kodi, hali iliyosababisha hasira toka kwa umoja wa wanahabari nchini Zambia na Serikali ya Marekani.

Mabadiliko ya katiba yaliyofanywa hivi karibuni, yanamaanisha kuwa mshindi ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, jambo ambalo ni wazi uwezekano wa kuwa na duru ya pili ya uchaguzi wa wagombea wawili pekee inawezekana.

Taifa hili ambalo ni koloni la zamani la Uingereza, ilitawaliwa na Kenneth Kaunda kuanzia mwaka 1964 hadi 1991 na kurekodi ukuaji wa pato ghafi GDP la asilimia 3.6 ikiwa ni kiwango kidogo zaidi cha ukuaji toka mwaka 1998.

Ukuaji wa uchumi ulikuwa zaidi ya asilimia 10 mwaka 2010, lakini kushuka kwa thamani ya madini ya shaba, madini ambayo nchi hiyo inategemea kwa kusafirisha nje, iliiweka nchi hiyo kwenye shinikizo kubwa, hii ni kwa mujibu wa shirika la fedha duniani IMF.
Zambia kupiga kura ya kumchagua Rais Alhamis hii Zambia kupiga kura ya kumchagua Rais Alhamis hii Reviewed by Bill Bright Williams on 12:09:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.