Updated Monday, August 1, 2016

Upinzani nchini Tanzania wasisitiza kufanya mikutano, Polisi waipiga marufuku


Polisi nchini Tanzania imesema haitaruhusu kufanyika kwa mikutano wala maandamano yoyote ya kisiasa ambayo yameitishwa nchi nzima na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo CHADEMA.

Jeshi la Polisi linasisitiza kuwa halitaruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa ambayo linasema huenda ikazua vurugu kwenye maeneo mengi ya nchi.

Haya yanajiri wakati Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, akiwaonya wanasiasa wa upinzani kutojaribu kutatiza hali ya amani inayoendelea kushuhudiwa nchini humo, na kuahidi kuwachukulia hatua wale wote watakaoshinikiza maandamano.

Mwishoni mwa juma akiwa ziarani kwenye mkoa wa Singida na Shinyanga, Rais Magufuli amesisitiza msimamo wake wa kutovumilia watu ambao wanamjaribu kwa kuitisha maandamano yasiyo na tija, huku akifafanua uamuzi wake wa kuzuia mikutano hiyo.

Rais Magufuli anasema hajakataza mikutano ya kisiasa wala kuminya demokrasia kama inavyodaiwa na viongozi wa upinzani, na badala yake, amesema mikutano ya wabunge na madiwani kwenye majimbo yao inaruhusiwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.

“Mimi niko tofauti na mtu asinijaribu kwa sababu nitamshughulikia” alisema Rais Magufuli mwishoni mwa juma wakati akionya kufanyika kwa maandamano na mikutano ya kisiasa iliyoitishwa na chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Mwishoni mwa juma mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alihojiwa kwa saa tatu na jeshi la Polisi, kutokana na matamshi aliyoyatoa juma moja lililopita kuwa chama chake kitaitisha mikutano na maandamano ya nchi nzima kuanzia tarehe Mosi ya mwezi Agosti.
Mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, akizungumza na wanahabari mara baada ya kiongozi wake kuachiwa kwa dhamana, amesema wanashangazwa na wito waliopewa na jeshi la Polisi, na kwamba sheria wanayoitumia haiendani na katiba ya nchi kwakuwa matamshi aliyoyatoa mwenyekiti wao, si ya kichochezi kama linavyodai jeshi la Polisi.

Hivi karibuni Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020 akisema kuwa muda wa kupiga kampeni na siasa umeisha baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wachambuzi wa mambo pia wanatofautiana kuhusu zuio la mikutano ya siasa, huku baadhi wakiunga mkono kauli ya Serikali na wengine wakipinga kwa madai kuwa uamuzi huo unarudisha nyuma demokrasia, huku wale wanaounga mkono wakidai kuwa muda wa siasa umeisha na badala yake wabunge na madiwani wafanye kazi kuwatumikia wananchi.

Usalama umeonekana kuimairishwa kwenye maeneo mengi ya nchi na hasa kwenye miji ambayo chama hicho kina wafuasi wengi.

Maandandamano haya hata hivyo hayajaungwa mkono na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo havipo kwenye muungano wa umoja wa Katiba ya wananchi UKAWA.

Upinzani nchini Tanzania wasisitiza kufanya mikutano, Polisi waipiga marufuku Upinzani  nchini Tanzania wasisitiza kufanya mikutano, Polisi waipiga marufuku Reviewed by Bill Bright Williams on 2:51:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.